UTANGULIZI

Kila sifa jema inamstahikia Allaah Aliyetukuka Muumba wa ulimwengu na walimwengu wake, Swalah na Salamu zimfikie kipenzi cha Waislamu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Sahaba zake kiraam (Radhiya Allaahu 'anhum) na kila anaewafuata kwa ihsaan mpaka Siku ya Mwisho.
Shari’ah, amri, makatazo na kanuni ni katika taratibu ambazo jamii haiwezi kiziepuka ikitaka kuwa na uadilifu, amani, usalama na uhuru kwa wana jamii wake. Jamii ni mchanganyiko wa wema, wabaya na kadhalika; hivyo huhitaji utaratibu wa kuwadhibiti, kuwazuia au kurekebisha na kuwatengeneza wale wenye kwenda kinyume na shari’ah ziliopo katika jamii ile; kwa kuwawekea adhabu, faini, fidia na kadhalika; lakini walio wema –raia wema- na wenye kufuata kanuni huwa hawana chao kitu, kwani hawawekewi –tunzo- kwa kufuata au kutunza kwao kanuni zaidi ya kuongezewa ushuru.
Uislamu ni mfumo kamili wa maisha kwa jamii, mfumo wenye kujitegemea usiohitaji mchango wa aina yo yote ile kutoka pahala popote pale katika jambo lolote lile; mfumo huo umekuja na mengi yakiwemo maamrisho na makatazo; shari’ah na kanuni; adhabu na malipo mazuri yasiyobagua baina ya kiongozi na mwenye kuongozwa; mfalme na raia; sharifu na dhaifu; tajiri na maskini; mweusi na mweupe, mwanamke na mwanamume na kadhalika; Qur-aan inasema:
“Na anayefanya mema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini; basi hao wataingia Jannah wala hawatadhulumiwa hata kadiri ya tundu ya kokwa ya tende” [An-Nisaa 4: 124]; kwa lengo la kuhakikisha kuwa wote wananufaika katika maisha yao ya duniani; na kwa wale Waumini wa Allaah na Siku ya Qiyaamah kutarajia malipo mema kutoka kwa Mola wao kwa kule kutekeleza kwao Amri Zake na kujikataza na Makatazo Yake bila ya kuendekeza au kufuata matamanio ya nafsi zao; kwa kuelewa na kuwa na yakini kuwa iymaan yao haikamili bila ya kumtii Mola wao na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Amri Zake na kujikatza na Makatazo Yake tena bila ya kuwa na khiari au uchaguzi katika Aliyoyahukumu kama isemavo Qur-aan:
“Haiwi kwa Muumini wa kiume wala Muumini wa kike Anapohukumu Allaah na Mjumbe Wake jambo wakawa wanakhiari –yakuchagua kinyume cha Alivyohukumu Allaah- katika jambo……” [Al-Ahzaab 33: 36].
Maamrisho na makatazo hayo yamekuja katika Qur-aan tukufu na katika Sunnah sahihi za Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); maamrisho au makatazo hayo huja na kumlenga mkusudiwa awe mwenye hadhi au cheo cha aina yoyote ile na adhabu yake haibagui kwa wenye kwenda kinyume na maamrisho awe sharifu au dhaifu; tajiri au maskini na kadhalika, kwani huko –kubagua kwa kuwaadhibi baadhi na kutokuwadhibu wengine- ni kuangamia kwa jamii kama tunavyoona katika ulimwengu wetu na kama alivyobainisha (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kusema:

“Kwa hakika waliangamia waliokuwa kabla yenu, wao walikuwa wakitekeleza al-hadd –adhabu- kwa wanyonge na wakiacha kuitekeleza kwa masharifu - waheshimiwa-; naapa kwa Yule Ambae nafsi yangu iko Mikono Mwake lau kama Faatwimah –binti Rassuli Allaahi- angelikuwa amefanya kosa –la kuiba- basi ningelimkata mkono wake.” [Imepokelewa naAl-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiri Qur-aan, Suuratul Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 6319 na 6320; naMuslim, katika Kitabu cha Huduud, mlango wa kumkata -mkono-mwizi sharifu na asiyekuwa sharifu na kukatazwa kushufaia katika Huduud, Hadiyth namba 3202.].
Kauli kama hii na nyingine nyingi zilizojaa katika mafundisho ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zinathibitisha na kuweka bayana kuwa Uislamu si utaratibu wa maisha uliowekwa na serikali/chama/kikundi fulani, bunge/wawakilishi; bali ni Shari’ah/Dini ya Allaah, Shari’ah/Dini ya kweli na ya Haki, kwani hata huyo aliyepewa huo ujumbe ambae ni Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ndie Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ndie kiongozi wa juu kabisa wa Uislamu wakati mwingine hujumuishwa na kuingizwa katika maamrisho au makatazo.
Mtume wetu mpenzi (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameamrishwa na kukatazwa kama ilivyo hali kwa wafuasi wake; kuna amri na makatazo yaliyomlenga yeye pekee yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama pele Allaah Aliposema:
Ee Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe Wake” [Al-Maaidah 5: 67].
Pia Allaah Anasema:
“Ee Mtume! Mche Allaah wala usiwatii makafiri na wanafiki” [Al-Ahzaab 33: 1].
Pia Allaah Anasema:
“Ee Mtume! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao…” [Al-Ahzaab 33: 59].
Pia Allaah Anasema:
“Ee Mtume! Kwa nini unaharamisha Alichokuhalilishia Allaah? Unatafuta kuwaridhisha wake zako…” [At-Tahriym 66: 1].
Pia Allaah Anasema:
“Wala usimswalie kabisa yeyote katika wao akifa, wala usisimame kaburini kwake” [At Tawbah 9: 84].
Wakati mwengine -na ndio kawaida ya Qur-aan- amri na makatazo huja kwa kumjumuisha Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtanguliza mbele ya wafuasi wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama pele Allaah Aliposema:
“Ee Nabii! Mtakapowapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Allaah, Mola wenu. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Allaah, msiikiuke…” [Atw-Twalaaq 65: 1].
Pia Allaah Anasema:
“Haimpasii Mtume na wale walioamini kuwatakia msamaha washirikina, ijapokuwa ni jamaa zao, baada ya kwisha bainika kuwa hao ni watu wa Motoni” [At-Tawbah 9: 113].
Pia Allaah Anasema:
”Allaah Hakujaalia mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake. Wala Hakuwafanya wake zenu - ambao mnawalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu - kuwa ni mama zenu. Wala Hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu hasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu tu. Na Allaah ndiye Anayesema kweli, naye ndiye Anayeongoa Njia. Waiteni kwa –majina ya- baba zao, huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Allaah ...” [Al-Ahzaab: 33: 4-5].
Pia maamrisho au makatazo hayo huja kwa ujumla na kwa makhsusi; kuna maamrisho au makatazo yenye kuwahusu watu wote –Waumini na wasio waumini- kama pale Allaah Anaposema:
“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu Aliyekuumbeni nyinyi na wale wa kabla yenu, ili mpate kuokoka.” [Al-Baqarah 2: 21].
Pia Allaah Anasema:
“Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate nyayo za shaytwaan…” [Al-Baqarah 2: 168].
Pia Allaah Anasema:
“Enyi watu! Hakika Ahadi ya Allaah ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala mdanganyifu asikudanganyeni juu ya Allaah” [Faatwir 35: 5].

No comments:

Post a Comment